Other News

Mafanikio ya Miaka 10 ya ZPRA

Nembo ya Mamlaka

zoezi la mtetemo

jengo la afisi ya ZPRA

2020-10-08  
UTANGULIZI

Mamlaka ya Udhibiti wa Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia (ZPRA) ni Taasisi iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria Nambari 6 ya Mwaka 2016 ya Mafuta na Gesi Asilia. Mamlaka hii ina jukumu la kusimamia na kudhibiti shughuli zote za Utafutaji, Uendelezaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar.
 
HISTORIA FUPI YA UTAFUTAJI WA MAFUTA NA GESI ASILIA ZANZIBAR

Utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia kwa Zanzibar  ulianza katika miaka ya 50 (1950’s) ambapo Kampuni za BP na Shell kwa pamoja zilifanya utafutaji huo katika Visiwa vya Unguja na Pemba. Utafutaji huo ulihusisha uchimbaji wa visima viwili vya nchi kavu kwa maeneo ya Zanzibar, kisima cha mwanzo (Zanzibar 1)  kilichimbwa Unguja mnamo mwaka 1956/57 katika eneo la Kama na kina urefu wa mita 4353. Kisima hicho kilionesha dalili ya uwepo wa viashiria vya Gesi Asilia.
Kisima cha pili (Pemba 5) kilichimbwa Pemba mnamo mwaka 1961/62  katika eneo la Tundauwa kikiwa na urefu wa mita 3886. Kisima hicho kilionesha dalili ya uwepo wa viashiria vya Mafuta na Gesi Asilia.


Kuanzia mwaka 1980 rasilimali ya Mafuta na Gesi Asilia ilikuwa inasimamiwa na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Shirika la Maendeleo la Mafuta na Gesi la Tanzania (TPDC) hadi pale ilipopitishwa Sheria nambari 21 ya Mafuta ya Tanzania ya mwaka 2015. Sheria hiyo imetoa fursa kwa  kila upande wa Jamhuri ya Muungano  wa Tanzania usimamie rasilimali hizo wenyewe.

Mnamo mwaka 2016, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilitunga Sheria ya Mafuta na Gesi Asilia ambayo ilianza kutumika rasmi mwezi Novemba 2016. Pamoja na mambo mengine, lengo kuu la Sheria hiyo ni kusimamia na kudhibiti kazi za Utafutaji, Uchimbaji, Uendelezaji na Uzalishaji wa Mafuta na Gesi Asilia kwa maeneo ya Zanzibar. Vile vile, kupitia Sheria hiyo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilianzisha taasisi mbili kwa ajili ya kusimamia sekta hiyo ambazo ni Mamlaka ya Udhibiti wa Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia (ZPRA) iliyoanzishwa mwezi Machi 2017 na Kampuni ya Uendelezaji wa Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar (ZPDC) iliyoanzishwa mwezi Juni 2018.
 
MUENDELEZO WA SHUGHULI ZA UTAFUTAJI WA MAFUTA NA GESI ASILIA ZANZIBAR

Shughuli za Utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia zilianza rasmi kupitia zoezi la uchukuaji wa taarifa kwa njia ya anga (FTG) mnamo mwezi Machi, 2017. Lengo la zoezi hili ni kuangalia uwepo wa miamba yenye uwezo wa kuhifadhi Mafuta na Gesi Asilia katika kitalu cha Pemba Zanzibar. Matokeo ya zoezi hilo yalisaidia kuendelea kwa zoezi jengine la Utafutaji kwa kutumia njia ya mtetemo (Seismic) zoezi hili lilifanyika kwa upande wa nchi kavu, bahari na kina kifupi cha maji (transitions zone) kwa maeneo ya visiwa vya Unguja na Pemba. Zoezi hilo lilianza rasmi mnamo mwezi Octoba, 2017 mpaka Febuari, 2019; madhumuni ya zoezi hilo ni kuangalia maumbile ya miamba yenye uwezo wa kuhifadhi rasilimali ya Mafuta na Gesi Asilia.
Baada ya kukamilika kwa zoezi la uchukuaji wa taarifa za mtetemo taarifa hizo zilipelekwa katika kituo cha Kampuni ya BGP kilichopo nchini Malaysia kwa ajili ya usafishaji (data processing).

KAZI KUU ZA MAMLAKA

1. Kufatilia na kudhibiti Utafutaji, Uendelezaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar
2. Kumshauri waziri anaehusika na Mafuta na Gesi Asilia juu ya kutoa, kuongeza muda, kusitisha na kufuta leseni ya Utafutaji, leseni ya Uendelezaji na kibali cha Uzalishaji wa Mafuta na Gesi Asilia.
3. Kutoa taarifa kwa Mamlaka husika kwa ajili ya ukusanyaji wa mrahaba, kodi na tozo zinazotokana na shughuli za Mafuta na Gesi Asilia.
4.  Kuishauri Serikali juu ya mipango endelevu, uendelezaji miundombinu, mipango ya hatua za mwisho na ukomo wa miundombinu iliyowasilishwa na Kampuni.
5. Kusimamia utekelezaji wa sheria, kanuni na masharti ya mikataba kwa Kampuni.
6. Kuhakikisha uanzishwaji wa kituo kikuu cha mfumo wa taarifa kwa watu wanaohusika na shughuli za Mafuta na Gesi Asilia, kusimamia taarifa za Mafuta na Gesi Asilia, kutoa taarifa na machapisho ya kila siku kuhusiana na Mafuta na Gesi Asilia. 
 
MAFANIKIO YA MAMLAKA (ZPRA)

Kusainiwa kwa Mkataba wa Mkataba wa Mgawanyo wa Uzalishaji wa Mafuta na Gesi Asilia – PSA kwa kitalu cha Pemba – Zanzibar
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanikiwa kusaini Mkataba wa Mgawanyo wa Uzalishaji wa Mafuta na Gesi Asilia – PSA kwa kitalu cha Pemba – Zanzibar mnamo tarehe 23 Oktoba 2018. Mkataba huo umeingiwa baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Kampuni ya RAK Gas ya Ras Al Khaimah kutoka UAE na kupelekea muendelezo wa shughuli mbali mbali za utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia katika kitalu cha Pemba -Zanzibar.

Kuwajengea uwezo  wafanyakazi kwa kuwapatia mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi kuhusiana na Mafuta na Gesi Asilia
 
Mamlaka ya Udhibiti wa Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia kupitia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanikiwa kuwapatia watendaji wa Mamlaka mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi katika fani mbali mbali za Mafuta na Gesi Asilia ili waweze kusimamia ipasavyo musuala hayo.
 
Kusimamia zoezi la Utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar kwa njia ya anga (Full Tensor Gradiometric Survey – FTGs) na njia ya mtetemo (2D Seismic Survey)

ZPRA imefanikiwa kusimamia kazi za utafiti zilizofanyika kuanzia mwezi Machi 2017 na kumalizika mwezi Aprili 2017 kwa zoezi la uchukuaji wa taarifa kwa njia ya Anga (Full Tensor Gradiometric Survey – FTGs) na kufuatiwa na kazi ya uchukuaji wa taarifa kwa njia ya mtetemo (2D seismic acquisition) ilioanza tarehe 28 Oktoba 2017 hadi tarehe 14 Februari 2019. Jumla ya mistari 101 ilifanyiwa utafiti katika maeneo ya baharini, nchi kavu na kina kifupi cha maji kwa eneo la Unguja na Pemba.
 
Kwa upande wa baharini, zoezi hilo lilianza tarehe 28 Oktoba 2017 na kukamilika tarehe 28 Novemba 2017 ambapo jumla ya mistari 66 ilichukuliwa taarifa katika zoezi hilo.
Kwa nchi kavu, zoezi la mtetemo lilianza tarehe 8 Februari 2018 hadi tarehe 25 Septemba 2018 ambapo jumla ya mistari 25 (Unguja 11 na Pemba 14) ilichukuliwa taarifa katika zoezi hilo.

Kwa maeneo ya kina kifupi cha maji, zoezi hilo lilianza tarehe 7 Disemba 2018 hadi tarehe 14 Februari 2019 ambapo jumla ya mistari 10 (Unguja 2 na Pemba 8) ilichukuliwa taarifa katika zoezi hilo.

Kufuatia kukamilika kwa zoezi la uchukuaji wa taarifa za mtetemo (2D seismic data acquisition) katika Kitalu cha Pemba - Zanzibar, taarifa hizo zilipelekwa katika kituo cha Kampuni ya BGP kilichopo Kuala Lumpur, Malaysia kwa ajili ya usafishaji na kufanyiwa tafsiri.
 
Kutoa Uelewa kwa Wananchi kuhusu Mafuta na Gesi Asilia
Mamlaka inaendelea kutoa uelewa katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba kuhusiana na shughuli za Mafuta na Gesi Asilia zinazoendelea kupitia Televisheni, Radio, Magazeti pamoja na kufanya mikutano na makongamano. Vile vile, Mamlaka inaendelea kutoa uelewa kwa wananchi na taasisi mbali mbali za Serikali na Binafsi kuhusu masuala ya Mafuta na Gesi Asilia.

Kutangaza Zabuni ya zoezi la uchukuaji wa taarifa kwanjia ya mtetemo ( Mult- Client 2D Seismic survey)
 
Kuendelea na matayarisho ya kufungua maeneo mapya ya kufanya Utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia kwa eneo la Zanzibar.
 
Mamlaka kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati, inaendelea na matayarisho ya kufungua maeneo mapya ya kufanya Utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia kwa maeneo ya kina kirefu cha maji kwa upande wa mashariki mwa Zanzibar.
 
Hadi sasa, Mamlaka ipo katika hatua ya kutafuta Kampuni itakayofanya zoezi la Pamoja la Uchukuaji wa Taarifa (Multi-client Survey) kwa njia ya zabuni.
Taarifa zitakazopatikana katika Zoezi hilo zitasaidia katika mgawanyo wa vitalu vipya (Graticulation) katika eneo la kina kirefu cha maji kwa ajili ya kuyafungua maeneo hayo na kuweza kutoa leseni kwa Kampuni za Utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia zitakazoridhiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
 
HITIMISHO

Mamlaka ya Udhibiti wa Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar inatoa shukurani kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kutoa kipaumbele katika sekta ya Mafuta na Gesi Asilia. Vile vile, Mamlaka inatoa shukurani kwa wananchi wote wa Zanzibar kwa kutoa ushirikiano wakati wote wa zoezi la Utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia.


 

Sign-up and we will notify you when there is news from DoEM